Home Habari Kuu Makali ya mafuriko: Wakazi wa Mombasa wapokea msaada

Makali ya mafuriko: Wakazi wa Mombasa wapokea msaada

0

Ilikuwa ni afueni kwa wakazi wa kaunti ya Mombasa ambao katika siku za hivi karibuni wamestahimili makali ya mafuriko yanayoshuhudiwa katika sehemu mbalimbali za nchi kufuatia mvua kubwa inayozidi kushuhudiwa. 

Mafuriko yamesababisha wakazi wengi katika kaunti hiyo kuachwa bila makazi huku mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa nchini ikiwataka Wakenya kujiandaa kwa hata mvua kubwa zaidi.

Leo Jumanne, Naibu wa Rais Rigathi Gachagua alizuru kaunti ya Mombasa na kutoa msaada wa chakula na bidhaa mbalimbali kwa waathiriwa wa mafuriko hayo.

Miongoni mwa walionufaika ni zaidi ya familia 1,000 zilizoathiriwa na mafuriko katika eneo la Kisauni.

Akizigawia familia hizo chakula kilichotolewa na serikali kuu, Gachagua alizitaka serikali za kaunti kuongeza usaidizi kwa waathiriwa wa mafuriko hayo.

Gachagua hususan aliitaka serikali ya kaunti ya Mombasa inayoongozwa na Gavana Abdulswamad Nassir kutenga na kutoa fedha za kupiga jeki juhudi za serikali kuu kukabiliana na athari za mafuriko katika jimbo hilo.

 

Website | + posts