Morocco ukipenda Atlas Lions watashuka dimbani Laurent Pokou kwa mchuano wa pili wa kundi F Jumapili jioni dhidi ya Chui wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC huku wakilenga ushindi ili kutinga raundi ya 16 bora.
Simba wa Atlas ambao wanaongoza kundi hilo kwa pointi 3 watafuzu kwa raundi ya 16 bora kujiunga na Senegal ikiwa watapata ushindi, huku DRC wakihitaji ushindi ili kuwa na matumaini ya kutinga raundi ya pili.
Pambano hilo litasimamiwa na refarii wa Kenya Dkt. Peter Waweru Kamaku.
Baadaye, Chipolopolo ya Zambia itakuwa na miadi dhidi ya Tanzania saa mbili usiku.
Zambia wana alama moja kutokana na mechi moja huku Tanzania maarufu kama Taifa Stars wakiwa bila pointi baada ya kunyukwa na Morocco.
Saa tano usiku,itakuwa zamu ya Afrika Kusini kupambana na Namibia katika derby ya COSAFA katika kundi E.
Bafana Bafana wanahitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kuingia raundi ya pili baada ya kushindwa na Mali wakati Brave Warriors wakisaka ushindi ili kufuzu kwa raundi ya 16 bora.