Home Habari Kuu Majaji wapya 25 wa mahakama kuu, 11 wa mahakama ya rufaa kuajiriwa

Majaji wapya 25 wa mahakama kuu, 11 wa mahakama ya rufaa kuajiriwa

0

Idara ya mahakama imenufaika pakubwa na mkutano kati ya mihimili mitatu ya serikali uliofanyika leo Jumatatu katika Ikulu ya Nairobi. 

Mkutano huo uliwaleta pamoja Rais William Ruto, Jaji Mkuu Martha Koome na Naibu wake Philomena Mwilu, Maspika wa bunge Moses Wetang’ula na Amason Kingi, Mwanasheria Mkuu Justin Muturi na mwenyekiti wa Baraza la Magavana Anne Waiguru miongoni mwa wengine.

Wakati wa mkutano huo, Rais Ruto na uongozi wa bunge waliridhia ombi la Jaji Koome la kutaka majaji zaidi kuajiriwa ili kuboresha utendakazi wa idara ya mahakama.

Ili kuhakikisha utoaji bora wa huduma na kuimarisha vita dhidi ya ufisadi, serikali kuu na bunge zilikubali kuunga mkono ombi la idara ya mahakama la kutengewa fedha zaidi ili kusaidia miongoni mwa mambo mengine kuajiriwa kwa majaji wapya 25 wa mahakama kuu na majaji wapya 11 wa mahakama ya rufaa.

“Rasilimali pia zitatolewa kuhitimisha mpango wa uazimaji wa magari ili kukidhi mahitaji ya uchukuzi ya idara ya mahakama,” ilisema taarifa kutoka kwa msemaji wa Ikulu ya Nairobi Hussein Mohamed.

Idara ya mahakama imekuwa ikilalamikia upungufu wa majaji katika hatua ambayo imesema imeathiri utendakazi na kusababisha mrundiko wa kesi.

Website | + posts