Home Kimataifa Mahakama yazima hatua ya serikali ya kuwapeleka polisi Haiti

Mahakama yazima hatua ya serikali ya kuwapeleka polisi Haiti

Jaji wa mahakama kuu Chacha Mwita, alisema baraza la usalama la kitaifa halina mamlaka ya kupeleka maafisa wa polisi kuhudumu nje ya nchi.

0
Mahakama yazima azma ya serikali ya kuwapeleka polisi nchini Haiti.
kra

Serikali imepata pigo jingine baada ya Mahakama kuu ya Kenya kusitisha hatua ya kupelekwa kwa maafisa wa polisi 1,000 nchini Haiti, ikisema hatua hiyo ni kinyume cha sheria.

Akitoa agizo hilo siku ya Ijumaa, jaji wa Mahakama Kuu Chacha Mwita, alisema baraza la usalama la kitaifa halina mamlaka ya kuwapeleka maafisa wa polisi kuhudumu nje ya nchi.

kra

Hatua ya kuwapeleka maafisa wa polisi nchini Haiti, ilipingwa mahakamani na Chama cha wanasheria nchini pamoja na kiongozi wa chama cha Thirdway Alliance Ekuru Aukot, ikitajwa kinyume cha katiba ya Kenya.

Katika uamuzi wake, Jaji Chacha Mwita alisema baraza la usalama la kitaifa limeruhusiwa tu kupeleka vikosi vya ulinzi KDF, kudumisha amani katika nchi za nje.

Kenya ilijitolea kuongoza kikosi cha maafisa wa polisi wa kimataifa kudumisha amani nchini Haiti mwezi Septemba mwaka 2023, baada ya Haiti kuomba msaada wa polisi wa  kimataifa, kurejesha hali ya utulivu nchini humo.

Waziri mkuu wa Haiti  Ariel Henry, alipohutubia baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, alisema serikali yake imezidiwa nguvu na magenge ya wahalifu, ambayo yanadhibiti asilimia 80 ya mji mkuu wa Port-au-Prince.

Website | + posts