Home Kimataifa Mahakama yatupilia mbali kesi dhidi ya Mkurugenzi Mkuu wa NTSA George Njao

Mahakama yatupilia mbali kesi dhidi ya Mkurugenzi Mkuu wa NTSA George Njao

Jaji huyo alisema mlalamishi alipaswa kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama wa hapo awali, badala ya kutuma ombi upya.

0
Mkurugenzi wa NTSA George Njao.
kra

Mahakama ya kushughulikia maswala ya wafanyakazi Jijini Nairobi, imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa ikitaka kuondolewa wadhifani kwa Mkurugenzi Mkuu wa halmashauri ya uchukuzi na usalama barabarani NTSA, George Njao.

Jaji Byram Ongaya aliamua kuwa ombi lililowasilishwa likitaka kuondolewa kwa Njao, ni mzaha kwa mchakato wa mahakama, akidokeza kuwa Mahakama hiyo hapo awali ilitoa maagizo katika swala hilo.

kra

Jaji huyo alisema mlalamishi alipaswa kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama wa hapo awali, badala ya kutuma ombi upya.

Aidha Justice Ongaya, alidokeza kuwa mlalamishi huyo kupitia wakili wake awali walikubali kusuluhisha swala hilo nje ya mahakama mnamo mwezi Januari mwaka 2023.

Hata hivyo mlalamishi Edwin Oduor alikanusha madai kwamba alikubali kutatua swala hilo nje ya mahakama.

“Ombi hili ni mzaha kwa mchakato wa mahakama. Mlalamishi alipaswa kukata rufaa iwapo hakukubaliana na uamuzi wa awali,” alisema Jusice Ongaya.

“Na kwa sababu mlalamishi amekiuka mchakato wa mahakama, atagharamia kesi hii,” aliagiza Jaji huyo.

Oduor alituma ombi kupinga kuongezwa muhula wa kuhudumu kwa Njao katika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa NTSA, akisema kuwa uteuzi wake haukuzingatia sheria na unapaswa kusimamishwa na mahakama.

Mlalamishi huyo pia alisema Njao alishindwa kutekeleza majukumu yake ipaswavyo wakati wa kipindi chake cha miaka mitatu, akitaja ongezeko za ajali za barabarani zilizosababisha maafa ya watu wengi.

Njao amehudumu wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa halmashauri ya NTSA tangu mwaka 2019, alipoteuliwa kwa muhula wa miaka mitatu.