Mahakama ya rufaa jijini Nairobi imetaja sheria ya fedha ya mwaka 2023 kuwa kinyume cha sheria.
Uamuzi huo wa leo Jumatano Julai 31, 2024 ulitolewa na jopo la majaji watatu wa mahakama ya rufaa ambao ni Kathurima M’Inoti, Agnes Murgor na John Mativo.
Kulingana na uamuzi huo, mahakama ilipata kwamba mchakato mzima wa kupitisha sheria ya fedha ya mwaka 2023 ulijaa makosa na kwamba ulikiuka maelekezo kadhaa ya katiba.
Sheria hiyo imebaikika kukiuka kifungu nambari 220 sehemu ya kwanza (a) na nambari 221 vya katiba ya Kenya pamoja na sehemu ya 37, 39A na 40 ya sheria ya usimamizi wa fedha za umma ambazo zinaainisha mfumo wa kutayarisha bajeti.
Majaji hao watatu waliamua kwamba kukosa kutimiza mahitaji ya sehemu hizo za katiba na sheria nyingine kunasababisha sheria nzima kuwa kinyume cha katiba.
Kosa kuu lililodhibitika katika mchakato wa kupitisha sheria ya fedha ya mwaka 2023 ni kukosa kuhusisha umma kikamilifu.
Kulingana na mahakama, bunge linawajibika kutoa sababu za kukubali au kukataa michango ya wakenya katika kuwahusisha kwenye uundaji wa sheria.
Bunge la kitaifa na bunge la seneti zinafaa kukubaliana katika uundaji wa sheria kama hizi na katika uundaji wa sheria hiyo mabunge hayo hayakukubaliana.
Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani na wanaharakati mbali mbali akiwemo seneta wa kaunti ya Busia Okiya Omtatah Okoiti.
Walitaka mahakama isimamishe utekelezaji wa sheria hiyo wakisema kwamba ilipitishwa bila kuzingatia maelekezo kadhaa ya katiba kama vile kushirikisha umma.
Hatima ya aina mbali mbali za ushuru zilizoanzishwa na sheria hiyo ya mwaka jana sasa haijulikani.