Home Kimataifa Mahakama yasimamisha kwa muda mgomo wa KUPPET

Mahakama yasimamisha kwa muda mgomo wa KUPPET

0

Mahakama ya ajira na mahuasiano ya Leba nchini imesimamisha kwa muda mgomo wa walimu wanachama wa chama cha KUPPET ambao wengi ni walimu wa shule za upili na vyuo.

Mgomo huo umesitishwa kutoa fursa kwa kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi iliyowasilishwa na tume ya kuajiri walimu nchini TSC Jumatatu ambapo wizara ya Leba imetajwa kama mhusika.

Katika uamuzi wake, Jaji James Rika alitoa maagizo ya kusitisha kwa muda mgomo wa KUPPET kulingana na matakwa ya TSC. Washtakiwa kwenye kesi hiyo wamezuiwa na mahakama kushiriki mgomo uliopangiwa kuanza Agosti 24, 2024.

Washtakiwa ambao ni wizara ya Leba na chama cha KUPPET wameagizwa pia kuwasilisha majibu yao kwa kesi hiyo katika muda wa siku saba na kesi hiyo itatajwa Septemba 5, 2024.

Chama cha KUPPET kilianzisha mgomo jana Jumatatu Agosti 26, 2024 baada ya serikali kukosa kutekeleza matakwa yao huku kile cha KNUT kikifutilia mbali mgomo ambao ungeanza siku hiyo hiyo ili kutoa fursa kwa mazungumzo.

Walimu wanachama wa KUPPET wameonekana katika sehemu mbali mbali za nchi wakiandamana barabarani huku wakizuru shule ambazo wenzao walifika kazini kwa lengo la kuwatoa humo ili wajiunge na mgomo.

Walimu wanataka awamu ya pili ya mkataba wa makubaliano ya pamoja itekelezwe, walimu wapandishwe vyeo, walimu wa JSS waajiriwe kwa masharti ya kudumu na warejeshewe bima ya afya.

Waziri wa elimu Julius Ogamba leo amesema kwamba serikali inaendeleza majadiliano na uongozi wa KUPPET ili kuafikiana kuhusu kusitishwa kwa mgomo guo.

Website | + posts