Home Habari Kuu Mahakama yakataa kusimamisha mazishi ya Kiptum

Mahakama yakataa kusimamisha mazishi ya Kiptum

Owuor anasema ana mtoto wa Kiptum wa umri wa mwaka mmoja na miezi saba na anahisi kwamba haki za mtoto huyo zitahujumiwa iwapo mazishi yake hayatasimamishwa.

0

Mahakama kuu ya Eldoret imekataa ombi la mwanamke mmoja anayetaka mazishi ya mwanariadha shupavu Kelvin Kiptum yasimamishwe kwa kile anachokitaja kuwa kutohusishwa kwenye mipango.

Edna Owuor wa umri wa miaka 22 kupitia kwa wakili wake Joseph Oyaro alitaka mahakama isimamishe maziko ya Kiptum akidai kwamba ana mtoto wake na hajahusishwa katika mipango ya mazishi.

Owuor anasema ana mtoto wa Kiptum wa umri wa mwaka mmoja na miezi saba na anahisi kwamba haki za mtoto huyo zitahujumiwa iwapo mazishi yake hayatasimamishwa.

Katika kukatalia mbali ombi hilo, jaji Robert Wananda alisema kwamba mipango ya mazishi ya Kiptum imekuwa ikiendelea kwa muda sasa na hela nyingi zimetumika na hivyo haitakuwa vyema kusimamisha shughuli nzima.

Owuor alitaka pia kuruhusiwa kuchukua sampuli za mwili wa mwendazake ili kufanikisha vipimo vya msimbojeni yaani DNA ili kudhibitisha kwamba yeye ndiye baba ya mtoto.

Ombi hilo pia halikukubaliwa na mahakama.

Kiptum na kocha wake waliangamia kwenye ajali ya barabarani Februari 11, 2024 saa tano usiku katika eneo la Kaptagat na mwili wake unatarajiwa kuzikwa kesho kwenye hafla ya kitaifa ambayo itahudhuriwa na Rais William Ruto.