Wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu vya umma nchini wameagizwa kusitisha mgomo wao hadi kesi iliyowasilishwa mahakamani kupinga mgomo huo itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Kesi hiyo imewasilishwa na Kongamano la Mashauriano kati ya Mabaraza ya Vyuo Vikuu nchini (IPUCCF) leo Jumatano dhidi ya Chama cha Wahadhiri (UASU).
Kesi hiyo itatajwa Oktoba 2 mwaka huu kwa lengo la kutoa maelekezo zaidi.
Jaji Dkt. Jacob Gakeri ameagiza vyuo vikuu na wahadhiri pamoja na wafanyakazi kuendelea kushiriki mazungumzo ili kuangazia malalamishi yaliyoibuliwa
Wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu vya umma wanashinikiza kutekelezwa kikamilifu kwa Mkataba wa Maelewano (CBA) wa mwaka 2021-2025 ambao miongoni mwa mambo mengine utawahakikishia nyongeza ya mishahara na kupandishwa vyeo.
Shughuli za masomo zilitatizika leo Jumatano kufuatia mgomo wa wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu ambao waliandamana na kuapa kutorejea kazini hadi matakwa yao yatimizwe.
Haijabainika ikiwa watatii agizo la mahakama la kuwataka kusitisha mgomo.