Home Habari Kuu Mahakama ya Rufaa yasitisha utozaji wa kodi ya nyumba

Mahakama ya Rufaa yasitisha utozaji wa kodi ya nyumba

0

Mahakama ya Rufaa imesitisha kodi ya nyumba wanayotozwa Wakenya ili kugharimia ujenzi wa nyumba za bei nafuu. 

Hii ni hadi masuala yote yaliyoibuliwa katika rufaa iliyowasilishwa na serikali ya kupinga uamuzi wa mahakama kuu kusitisha utozaji wa kodi hiyo yatakaposikizwa na kuamuliwa.

Katika uamuzi wao, majaji Lydiah Achode, John Mativo and Gachoka Mwaniki wa Mahakama ya Rufaa walisema haitakuwa vyema baadhi ya Wakenya kutozwa kodi hiyo ambayo ilitajwa na Mahakama Kuu katika uamuzi wake kuwa kinyume cha katiba.

“Mahakama Kuu ilishikilia kuwa kodi ya nyumba ilianzishwa bila mpangokazi wa kisheria. Pia ilishikilia kuwa kodi hiyo iliwalenga baadhi ya Wakenya. Katika mtazamo wetu, maslahi ya umma yamejikita katika kusubiri kuamuliwa kwa rufaa hiyo,” walisema majaji Achode, Mativo na Mwaniki katika uamuzi wao.

“Hii kwa sababu ikiwa ombi la kutaka kodi hiyo iendelee kutozwa litatolewa kwa wakati huu, ikiwa Mahakama ya Rufaa itakubaliana na uamuzi huo, basi baadhi ya maamuzi makubwa ambayo yatakuwa yamefanywa kuhusiana na sheria husika huenda yasiweze kubatilishwa.”

Kodi ya nyumba ilianza kutozwa baada ya kutekelezwa kwa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2023 mwezi Juni mwaka jana.

Fedha zinazopatikana kupitia utozaji wa kodi hiyo zinatumiwa kufadhili ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kote nchini.

Rais William Ruto ameapa kuwa hakuna kitakachozuia ujenzi wa nyumba za gharama nafuu anaosema utahakikisha Wakenya wasiojiweza kiuchumi wanamiliki nyumba.