Home Habari Kuu Mahakama ya Makadara kufungwa kwa wiki nyingine moja

Mahakama ya Makadara kufungwa kwa wiki nyingine moja

0
Jaji Mkuu Martha Koome (kulia) Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu (katikati) na Msajili wa idara ya Mahakama Winfridah Mokaya (Kushoto).
kra

Jaji Mkuu Martha Koome ametangaza kwamba mahakama ya Makadara itaendelea kufungwa kwa muda wa juma moja zaidi.

Kwenye taarifa, Koome ambaye pia ni Rais wa Mahakama ya Upeo nchini aliainisha shughuli ambazo zitaendelea katika mahakama hiyo kuanzia leo, Juni 24, 2024 hadi shughuli za kawaida zitakaporejelewa Julai Mosi, 2024.

kra

Kuanzia leo hadi Jumatano, utakuwa muda wa kutathmini athari za kisaikolojia za kisa cha kupigwa risasi kwa Hakimu Mkuu Monica Kivuti kwa wote wanaofanya kazi katika mahakama ya Makadara ambapo pia watapokea huduma za ushauri nasaha.

Alhamisi, Juni 27, 2024, kamati ya watumizi wa mahakama itakutana kujadili jinsi ya kurejelea kazi katika mahakama hiyo na kutathmini hatua za usalama ambazo zimewekwa kufikia sasa.

Ijumaa 28, Juni, 2024 ni siku ya kudurusu daftari za miadi ya mahakama na kuweka tarehe mpya za kusikilizwa kwa kesi mbalimbali zilizokuwa zikiendelea kwenye mahakama ya Makadara, kabla ya kurejelea shughuli Julai Mosi.

Kwa sasa, kesi zilizokuwa zinaendelea katika mahakama ya Makadara na ambazo haziwezi kuahirishwa zimeelekezwa katika mahakama ya Milimani.

Jaji Mkuu aligusia pia hatua za kiusalama ambazo zimewekwa katika vituo vyote vya mahakama nchini ambapo wote watakaoingia kwenye vituo hivyo watafanyiwa uchunguzi ili kuzuia watu kuingia humo na silaha.

Wafanyakazi katika vituo hivyo watatakiwa kuvaa kadi zao za utambuzi kila wakati na magari yatakayoegeshwa katika vituo hivyo ni lazima yawe na vibandiko maalumu.

Idadi ya wateja watakaoruhusiwa kufika kwenye afisi za majaji, mahakimu na watendakazi wengine wa mahakama itapunguzwa pakubwa huku madawati ya kuhudumia wateja yakiwezeshwa kidijitali ili kupunguza msongamano.

Haya yanajiri kufuatia kisa cha kupigwa risasi kwa Hakimu Kivuti katika mahakama ya Makadara. Kivuti baadaye aliaga dunia kutokana na majeraha aliyopata na tayari amezikwa nyumbani kwake katika eneo la Yatta, kaunti ya Machakos.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here