Home Kaunti Mahakama ya Gichugu yashirikiana na umma kupunguza mrundiko wa kesi

Mahakama ya Gichugu yashirikiana na umma kupunguza mrundiko wa kesi

0
Hakimu mwandamizi wa mahakama ya Gichugu Leah Kibaria.
kra

Mahakama ya Gichugu  imezindua mpango wa “Kutana Na Mahakama” unaolenga kuhamasisha umma mashinani kuhusu utumizi wa njia mbadala zakutatua kesi, ili kupunguza mrundiko wa kesi mahakamani.

Hakimu Mwandamizi wa mahakama ya Gichugu Leah Kibaria, alisema tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi mwezi Julai, kesi 800 zaidi zimesajiliwa, huku kesi 1,400 zikiwa bado hazijashughulikiwa.

kra

kulingana na hakimu huyo, kesi 800 zaidi huenda zikasajiliwa katika kipindi ambacho kimesalia mwaka huu na hivyo ipo haja kukumbatia mbinu mbadala za kutatua kesi, ili kuzuia uharibifu wa rasilimali.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo mjini Kiamutugu, Gichugu, Kibaria alisema wamejizatiti kuwahamasisha wananchi kutumia mbinu mbadala za kutatua migogoro.

“Kuanzia mwaka huu hadi mwezi Julai, tumesajili kesi 800 zaidi, deta zetu zinaashiria kuwa kesi 1,400 bado hazijashughulikiwa na tunatarajia kesi 800 zaidi zitasajiliwa kufikia mwezi Disemba,” alisema Kibaria.

Kibaria aliongeza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha kesi zinaamuliwa katika muda mfupi zaidi.

“Sisi sote hukiuka sheria maishani mwetu. Tunapaswa kukubaliana jinsi ya kutatua mizozo kwa kutumia rasilimali chache,” alisema hakimu huyo.

Mpango huo utaenezwa katika mahakama zingine za Kirinyaga ili kufanikisha upatikanaji wa haki.