Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) imerejelea vikao vyake juma hili mjini Arusha Tanzania, baada ya kufungwa tangu mwezi Mei mwaka huu kwa kukosa pesa.
Majaji walianza kutekeleza majukumu yao tarehe 16 mwaka huu, huku wakilenga kumaliza mrundiko wa kesi ifikiapo Oktoba 11.
Zaidi ya kesi 260 hazijatatuliwa kutokana na kusitishwa kwa vikao.
Kesi zilizowasilishwa ni za kutoka kwa mataifa wanachama ya Tanzania,Uganda na Kenya.
Kikao cha sasa cha mahakama hiyo kitaenda hadi tarehe 11 mwezi ujao ambapo inatarajiwa kuskiza kesi 25,zikiwemo kuamua 15 kati ya hizo na nyingine zilizopendekezwa kutoka kwa mahama mengine ya mataifa wanachama.
Mojawapo ya kesi ambayo imeratibiwa kuskizwa Septemba 24 ni ile iliyowasilishwa na kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua kupinga hatua ya tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC, kumntangaza Rais William Ruto, kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa Urais mwaka 2022.
Karua pia ameshtaki mahakama ya upeo ya Kenya kwa kushindwa kufanya maamuzi yafaayo katika kesi ya kupinga matokeo ya Urais.
Kesi nyingine mbele ya mahakama hiyo ni ile ya mzozo wa mpaka kati ya Rwanda na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo.