Home Habari Kuu Mahakama: Paul Mackenzie na wenzake walazwe hospitalini

Mahakama: Paul Mackenzie na wenzake walazwe hospitalini

Mahakama  hiyo imeamuru kwamba Mackenzie na wenzake walazwe hospitalini, baada ya kuanza kususia chakula wakiwa kizuizini.

0
Mhubiri wa kanisa la Good News International, Paul Mackenzie.

Mhubiri tata Paul Mackenzie na washukiwa wengine wenza 94 wataendelea kuzuiliwa gerezani hadi Machi 5, 2024.

Mahakama  imeamuru kwamba Mackenzie na wenzake walazwe hospitalini baada ya kuanza kususia chakula wakiwa kizuizini.

Hakimu Mwandamizi wa Mahakama Kuu Alex Ithuku anatarajiwa kutoa mwelekeo kuhusu uamuzi wa ombi la dhamana lililotolewa wiki iliyopita na mawakili wao Wycliffe Makasembo na Lawrence Obonyo.

Mackenzie na washirika wake walifika mahakamani siku ya Jumanne kwa ajili ya kusikilizwa kwa dhamana yao huku wakiwa wanyonge na hata wengine wakihitaji usaidizi wa viti vya magurudumu.

Wakili Makasembo aliambia mahakama kwamba wateja wake walikuwa wamesusia kula chakula kulalamikia mapokezi duni wanayoendelea kupata wakiwa gerezani.

Mawakili wa upande wa mashtaka, hata hivyo, walipinga hatua ya kuachiliwa kwa washukiwa hao kwa dhamana kwa misingi kwamba huenda wakatoroka nje ya nchi.

Wakili wa upande wa mashtaka pia alitaja uwezekano wa kuhitilafiana na mashahidi.

Washukiwa hao wanakabiliwa na makosa 238  ya mauaji yanayohusiana na maafa ya Shakahola yaliyoshuhudiwa mwaka uliopita.

Website | + posts