Home Burudani Mahakama kuu yazuia KECOBO kugawa mapato ya vyombo vya kubebea muziki

Mahakama kuu yazuia KECOBO kugawa mapato ya vyombo vya kubebea muziki

0
kra

Bodi ya hakimiliki nchini Kenya KECOBO imezuiwa na mahakama kuu kugawa mapato yaliyotokana na ushuru wa vyombo vya kubebea muziki ambavyo havijatumiwa.

Hii ni baada ya mwimbaji wa nyimbo za injili Reuben Kigame kupinga utekelezaji wa ushuru huo mahakamani.

kra

Jaji Lawrence Mugambi aliagiza kwamba ugavi wa mapato hayo kwa mashirika mengine yanayohusika na sanaa na hakimiliki ambayo ni MCSK, PRISK na KAMP usitishwe hadi kesi hiyo isikilizwe na kuamuliwa.

Alitaja suala hilo kuwa la dharura akisema litatajwa mahakamani Oktoba 16, 2023.

Katika kesi hiyo iliyowasilishwa na Kigame na wengine wawili, walioshtakiwa ni bodi ya hakimiliki nchini KECOBO, mtandao wa wanabiashara nchini – Kenya Trade Network, mamlaka ya kukusanya ushuru nchini KRA, Waziri wa michezo na sanaa na mwanasheria mkuu.

KECOBO ilistahili kuanza kugawa pesa hizo kwa mashirika mengine ya wasanii baada ya kutangaza utekelezaji wa ushuru huo kuanzia Septemba 15, 2023.

Ushuru huo unatozwa vyombo vya kubebea muziki na hata filamu vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi na hulipwa katika viingilio vya humu nchini.

Akizungumza kwenye mahojiano na kipindi cha Tamrini cha runinga ya KBC jana mkurugenzi mtendaji wa shirika la hakimiliki za wanamuziki nchini MCSK, Ezekiel Mutua alielezea kwamba dhamira ya ushuru huo ni kuongezea wasanii mapato.

Website | + posts