Home Kimataifa Magenge yavamia gereza na kuachilia wafungwa Haiti

Magenge yavamia gereza na kuachilia wafungwa Haiti

0

Magenge yaliyojihami yamevamia gereza kuu la Haiti katika jiji kuu Port-au-Prince na kauchilia wafungwa wapatao elfu 4.

Wanachama wa magenge hayo waliokuwa wamezuiliwa kuhusiana na mauaji ya Rais Jovenel Moïse mwaka 2021 ni kati ya waliotoroka kutoka kwenye gereza hilo.

Vurugu zimekuwa zikiongezeka nchini haiti katika miaka ya hivi karibuni ambapo magenge hayo yanalenga kumbandua mamlakani waziri mkuu Ariel Henry.

Yanadhibiti sehemu kubwa ya jiji la Port-au-Prince.

Vurugu za hivi punde zilianza Alhamisi wakati waziri huyo mkuu alikuwa safarini Nairobi Kenya kwa ajili ya majadiliano kuhusu kutumwa kwa kikosi cha maafisa wa usalama kinachoongozwa na Kenya nchini humo.

Kiongozi wa mojawapo ya magenge hayo kwa jina Jimmy Chérizier almaarufu “Barbecue” alitangaza kwamba watashirikiana katika shambulizi lililopangwa kuondoa waziri huyo mkuu mamlakani.

Chérizier ambaye aliwahi kuhudumu kama afisa wa polisi alisema magenge yote katika miji mbali mbali yana umoja.

Ufyatulianaji risasi ulishuhudiwa wakati wa uvamizi huo wa gereza kuu ambapo maafisa wanne wa polisi waliuawa huku watano wakipata majeraha.

Ubalozi wa Ufaransa nchini Haiti tayari umeshauri raia wake dhidi ya kusafiri kuingia au kutoka katika jiji la Port-au-Prince.

Uvamizi huo ulitekelezwa Jumamosi jioni na kufikia jana Jumapili lango la gereza hilo bado lilikuwa wazi na maafisa hawakuonekana huku miili ya wafungwa watatu waliouawa wakati wa kisa hicho ikiwa kwenye bustani.

Hata hivyo wafungwa wengine wapatao 99 wakiwemo wanajeshi wa zamani wa Colombia waliofungwa kuhusiana na mauaji ya Rais Moïse, waliamua kusalia kwenye seli zao wakihofia kuuawa kwenye makabiliano.

Website | + posts