Home Taifa Magavana wapinga KRA kutoza ushuru mapato ya kaunti

Magavana wapinga KRA kutoza ushuru mapato ya kaunti

0

Magavana wamelalamikia vikali matakwa ya Mamlaka ya Ukusanyaji Mapato nchini, KRA ya kutaka kutoza vyanzo mbalimbali vya mapato ya serikali za kaunti ushuru thamani wa ziada, VAT. 

Katika taarifa iliyotolewa kupitia mwenyekiti wa Baraza la Magavana Anne Waiguru, Magavana hao wamesema matakwa ya KRA yanaenda kinyume cha kanuni za Kifungu 6(2) cha Katiba ya nchi.

“Kifungu 209 cha Katiba kinaelezea ushuru na matozo yanayopaswa kutozwa na serikali kuu na serikali za kaunti. Kwa hivyo, tunaona matakwa ya KRA ya kutoza VAT kwa mapato yanayokusanywa na kaunti kuwa kinyume cha katiba na kuwa mwingilio wa mamlaka ya kaunti ya kutoza kodi kinyume cha Kifungu 209(3) na (4) cha Katiba,” alisema Waiguru ambaye pia ni Gavana wa kaunti ya Kirinyaga.

“Kwa hivyo tunadumisha kuwa Katiba ya nchi haikudhamiria serkali kuu kutoza ushuru mapato yanayokusanywa na serikali za kaunti.”

Magavana sasa wanaitaka KRA kukoma kutoa matakwa hayo wanayosema hayana msingi wa kisheria.

Matamshi yao yanakuja wakati ambapo KRA imeongeza jitihada za kutumia kila mbinu kuongeza mapato yanayokusanywa na serikali kuu kwa lengo la kufadhili miradi mbalimbali.

Ni kwa sababu ambapo Mswada wa Fedha 2024 umekumbana na pingamizi kwa kile wakosoaji wake wanasema utafanya gharama ya maisha kupanda hata zaidi.

Kupitia mswada huo, KRA inapania kukusanya takriban shilingi bilioni 300 kupitia ukusanyaji ushuru ikiwa utapitishwa.

 

 

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here