Home Habari Kuu Magavana wakongamana Narok kuangazia ugatuzi

Magavana wakongamana Narok kuangazia ugatuzi

0

Baraza la magavana nchini limeanza kongamano la siku mbili katika mbuga ya Maasai Mara, kaunti ya Narok kuangazia hali ya ugatuzi, mwaka mmoja baada ya kuanza kwa awamu ya tatu ya ugatuzi.

Kulingana na mwenyekiti wa baraza hilo Ann Waiguru gavana wa kaunti ya Kirinyaga, lengo la mkutano huo ni kutathmini kuhusu mapungufu, mazuri, fursa na vitisho vya ugatuzi na kuamua kwa kauli moja kuhusu namna ya kuimarisha ugatuzi.

Magavana hao wataamua kwa pamoja kuhusu jinsi ya kuhusiana na wadau wengine wa ugatuzi kama serikali kuu, wanaharakati na sekta ya kibinafsi.

Viongozi hao wa kaunti watajadiliana pia kuhusu majukumu yao na majukumu ambayo hayajatimizwa na yanafaa kuhamishiwa kaunti pamoja na kutafuta raslimali kutoka kwa washirika wa maendeleo, serikali kuu, mgao na mikopo.

Waiguru alishukuru gavana wa kaunti ya Narok Patrick Ntutu kwa kuwa mwenyeji wao katika mbuga hiyo maarufu ya kitaifa.

Naibu mwenyekiti wa baraza la magavana aliye pia gavana wa Wajir Ahmed Abdulahi alisema wataangazia madhara ya mvua kubwa inayoshuhudiwa katika maeneo ya Kaskazini Mashariki na Pwani.

Gavana wa Nandi Stephen Sang alisema wataungana na gavana wa mazingira na misitu Soipan Tuya ambapo watapanda miti kama njia ya kuongoza kwa vitendo.

Website | + posts