Home Kaunti Magari ya kibinafsi yapigwa marufuku kuingia Maasai Mara

Magari ya kibinafsi yapigwa marufuku kuingia Maasai Mara

0

Serikali ya kaunti ya Narok imepiga marufuku utumizi wa magari ya kibinafsi kuingia katika hifadhi ya wanyamapori ya Maasai Mara.

Msimamizi Mkuu wa Hifadhi hiyo Alex Nabaala, amesema maagizo hayo yanafuata mipango mapya ya kuedeleza shughuli za Maasai Mara, yaliyotiwa saini kuwa sheria mwaka jana. Nabala pia amesema magari yatakayoruhusiwa kuingia katika hifadhi hiyo ni magari ya Safari ambayo yameidhinishwa.

Gavana wa Narok Patrick Ole Ntutu, pia alitoa taarifa kuhusu agizo hilo akithibitisha kuwa magari ya kibinafsi hayatatumika tena ndani ya hifadhi hiyo kutokana na kelele na mikusanyiko isiyoidhinishwa ambayo imekuwa ikiendelea ndani ya Maasai Mara.

Kulingana na Gavana huyo, watumizi wa magari ya kibinafsi wamekuwa wakionyesha utovu wa nidhamu ndani ya hifadhi hiyo wakipuuza kanuni za hifadhi na kuhatarisha maisha yao.

Wengi wa watumizi wa magari ya kibinafsi kwenye hifadhi ya Maasai Mara wamekuwa wakitumia chaguo hilo ili kupunguza gharama ya kukodisha magari ya safari.

Magari yote ya kibinafsi sasa yatalazimika kuegeshwa nje ya lango la Sekenani, jambo ambalo litalazimu wanaozuru hifadhi hiyo kulipa zaidi ili kupata magari yalioidhinishwa kuingia katika hifadhi hiyo pamoja na gharama ya ziada kuwalipa waongoza watalii.