Home Kimataifa Mafuriko Manyara: Serikali ya Tanzania yasema watu zaidi ya 50 wamefariki

Mafuriko Manyara: Serikali ya Tanzania yasema watu zaidi ya 50 wamefariki

0

Serikali ya Tanzania imetangaza kuwa itagharimia mazishi ya zaidi ya watu 50 ambao wamepoteza maisha yao kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo katika eneo la Katesh wilayani Hanang mkoani Manyara.

Watu wengine zaidi ya 80 wamejeruhiwa na Rais Samia Suluhu ameagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhakikisha kwamba wanatibiwa kwa gharama ya serikali.

Waliojeruhiwa wamekuwa wakipatiwa matibabu na kuruhusiwa hali zao zinapokuwa zimeimarika na wengine wamekuwa wakipelekwa hospitali kwa ajili ya kupata matibabu na kuondoka.

Taarifa zinasema kuporomoka kwa sehemu ya Mlima Hanang ndio chanzo cha mafuriko hayo.

Mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia jumapili imesababisha mafuriko ya tope zito katika eneo hilo.

Akizungumza na wanahabari, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema eneo kubwa lililoathirika na mafuriko hayo ni kata ya Gendabi katikati ya mji wa Katesh.

Bi. Sendiga ameiambia BBC kwamba Serikali imeongeza juhudi za kufukua vifusi kuondoa miili katika tope zito.

”Kitu kama hiki kinapotokea cha ghafla watu hukimbia kimbia, mwingine anakwambia simuoni mtoto wangu, hapa hajaonekana, kwahiyo tulichofanya kwanza tumejaribu kupita kule kwenye eneo ambalo changamoto ilianzia na tumewaambia wapite hospitali kuangalia miili iliyo hospitalini na wagonjwa waliolazwa huko” Alisema.

Kikosi cha kupambana na maafa chini ya Ofisi ya Waziri mkuu kimetumwa Katesh kufanya shughuli mbalimbali za uokoaji ambapo tayari kambi tatu zimeandaliwa kwa ajili ya kuwapatia hifadhi watu waliokosa kabisa mahali pa kuishi.

‘’Kikosi maalumu cha jeshi kimetumwa usiku kusaidia kuopoa miili iliyokwama katika tope na kurejesha miundo mbinu katika hali yake ya kawaida’’

Aidha Wananchi wamesisitizwa kuhama katika maeneo hatarishi ikiwemo chini ya milima na katika maeneo ya mabonde.

Imeandikwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Seif Abdallah.

BBC
+ posts