Home Habari Kuu Mafunzo ya magonjwa yanayohusiana na tabia nchi yatolewa kwa wahudumu wa afya...

Mafunzo ya magonjwa yanayohusiana na tabia nchi yatolewa kwa wahudumu wa afya Wajir

0

Wafanyakazi wa afya katika kaunti ya Wajir kwa sasa wanapewa mafunzo ya siku tano yanayolenga kuwaongezea ujuzi kuhusiana na namna ya kufanya uangalizi na usimamizi wa magonjwa yanayohusiana na tabia nchi.

Mafunzo hayo yameandaliwa kutokana na usaidizi wa kiufundi na kifedha kutoka kwa Shirika la Afya Duniani, WHO.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, mafunzo hayo yanakusudia kuongeza uwezo wa maafisa hao wa afya kutibu magonjwa na kuangalia dalili za magonjwa hayo hasa magonjwa yanayohusiana na tabia nchi na dharura zinazoweza kutokea.

“Kufuatia ukame wa muda mrefu, hali hiyo inayoweza kutokea inaongeza hatari ya kutokea kwa magonjwa yanayoenezwa kupitia maji machafu na yanayoambukizwa na wadudu kama vile malaria, kipindupindu na kidingapopo. Dhamira yetu isiyoyumba ni kuhakikisha timu zetu za kuwahudumia wagonjwa zimejiandaa ipasavyo kukabiliana na changamoto hizi zinazotarajiwa kutokea,” imesema Wizara ya Afya katika taarifa.