Serikali ya kaunti ya Nairobi inapanga kuzindua maeneo 6 ya kiutawala kwa lengo la kugatua huduma za serikali.
Kaunti zote ndogo 17 za kaunti ya Nairobi zimepangwa kwenye maeneo hayo 6 ya kitawala ambayo ni Eneo la kati (Central), eneo la mashariki (Eastern), eneo la Magharibi (Western), eneo la Kaskazini (Northern), eneo la Kusini (Southern) na eneo la Kaskazini Mashariki (South Eastern).
Eneo la kati linajumuisha kaunti ndogo za Mathare, Kamukunji na Starehe, eneo la Mashariki lina kaunti ndogo za Embakasi ya kati, ya magharibi na ya Kaskazini, huku eneo la Magharibi likijumuisha kaunti ndogo za Dagoretti Kaskazini na Dagorreti Kusini.
Eneo la Kaskazini lina kaunti ndogo za Ruaraka, Roysambu na Kasarani, Eneo la Kusini lina kaunti ndogo za Kibra na Lang’ata na eneo la Kusini Mashariki lina kaunti ndogo za Embakasi Kusini, Embakasi Mashariki na Makadara.
Kila eneo litasimamiwa na meneja na mpango wa maendeleo utakuwa mmoja, bajeti moja katika kila eneo.
Mwaka jana serikali ya kaunti ya Nairobi ilibuni kamati ya kiufundi ya kuendesha mpango wa kubuni maeneo hayo ya kiutawala na kamati hiyo ilitekeleza ushirikishaji wa umma mwezi Novemba mwaka jana.
Awali pendekezo lilikuwa la maeneo matano na baada ya shughuli ya kushirikisha umma, kamati hiyo ikaamua maeneo yawe 6.