Home Habari Kuu Maelfu ya Wakenya kunufaika na ajira za ughaibuni

Maelfu ya Wakenya kunufaika na ajira za ughaibuni

Kenya pia itapeleka wafanyikazi 20,000 nchini Serbia kuhudumu katika sekta za ujenzi na utoaji huduma.

0

Saudi Arabia imetangaza nafasi 2,500 za ajira kwa wauguzi na wahudumu wengine wa afya waliohitimu humu nchini.

Kwenye taarifa, msemaji wa ikulu Hussein Mohamed, amesema hatua hiyo inatokana na juhudi za Rais William Ruto za kushauriana na washirika wa kimataifa katika kujadili mikakati ya kuwatafutia Wakenya fursa za ajira duniani.

Mohamed alitangaza kwamba nafasi zingine 310,000 za ajira kwa Wakenya kuhudumu katika mataifa ya kigeni, zinasubiri kuidhinishwa katika nchi nne.

Alisema mikataba ya ajira inayoendelea itakapokamilishwa, Kenya itaruhusiwa kuwapeleka wafanyakazi 250,000 Ujerumani na wengine 30,000 nchini Israel ili kufanya kazi katika sekta ya kilimo huku nafasi 3,000 zikitarajiwa kuwa wazi kufikia mwezi Machi mwaka huu.

Kenya pia itapeleka wafanyakazi 20,000 nchini Serbia kuhudumu katika sekta za ujenzi na utoaji huduma huku wengine 10,000 wakipelekwa nchini Urusi.

Msemaji huyo wa ikulu alikariri kujitolea kwa Rais Ruto kukuza Kenya kuwa kivutio cha uwekezaji, utengenezaji bidhaa, biashara, na utalii, pamoja na kuikuza kuwa kitovu cha wafanyakazi waliohitimu duniani.