Maelfu ya Wakenya wamejitokeza katika bustani ya Uhuru Gardens kunakoandaliwa sherehe za kuadhimisha miaka 60 tangu Kenya ilipojinyakulia uhuru miaka 60 iliyopita.
Rais William Ruto ataongoza sherehe hizo zitakazohudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka nje ya nchi.
Rais Ruto tayari amewasili katika bustani hiyo na anatarajiwa kutumia fursa hiyo kuangazia hatua ambazo Kenya imepiga tangu ijiatie uhuru.
Naibu Rais Rigathi Gachagua, Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, Mawaziri, Maspika wa bunge la Kitaifa na Seneti na viongozi wakuu serikalini tayari wamewasili katika bustani ya Uhuru Gardens kuhudhuria sherehe hizo.
Wakenya wengi walianza kuwasili katika uwanja huo leo Jumanne asubuhi na mapema huku baadhi wakiwa wamevalia mavazi yaliyo na bendera ya kitaifa ili kudhihirisha uzalendo wao.
Katika mtandao wa Google, bendera ya Kenya pia ilipepea kudhihirisha ulimwengu unajiunga na Kenya kuadhimisha siku hiyo.
Marais wa Aleksandr Lukashenko Belarus, Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Sahle Work Zewde wa Ethiopia ni miongoni mwa viongozi watakaohudhuria sherehe hizo.
Rais wa Ethiopia na ujumbe wake walilakiwa jana Jumatatu katika uwanja wa ndege wa kitaifa wa Jomo Kenyatta na Waziri wa Biashara na Viwanda Rebecca Miano.
Awali, Rais Lukashenko alifanya mazungumzo na Rais Ruto katika Ikulu ya Nairobi, ambapo viongozi hao wawili walikubaliana kuboresha uhusiano wa nchi hizi mbili hasa katika sekta za nishati, biashara, uwekezaji na elimu.