Makumi ya maelfu ya raia wa Israel wamejitokeza barabarani mapema Jumapili kumshinikiza Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kutia saini makubaliano yatakayowezesha kuachiliwa huru kwa Waisraeli walioshikwa mateka katika Ukanda wa Gaza.
Yamkini watu laki saba na nusu walifurika katika barabara za mji mkuu Tel Aviv na Haifa kushikiniza kuachiliwa huru kwa mateka hao.
Raia nchini Israel wanataka serikali isitishe mashambulizi katika Ukanda wa Gaza ili wenzao waliotekwa nyara waachiliwe huru.
Hii inafuatia kupatikana kwa miili sita ya mateka wa Israel, hali iliyowakera wananchi wanaomtaka Netanyahu kulegeza msimamo wake.
Kundi la Hamas liliwaachilia mateka 105 mwezi Novemba mwaka jana baada ya maafikiano, huku kundi hilo la waasi likitaka serikali ya Israel iwaachilie huru wafungwa Wakipalestina walio kwenye magereza nchini Israel, kubadilishana na mateka wa Israel wanaowashikilia.
Pendekezo hilo limekatiliwa mbali na Netanyahu.
Inakisiwa zaidi ya Waisraeli 100 wametekwa nyara, wengi wao wakiaminika kuawa.
Majeshi ya Israel yamewaua zaidi ya Wapalestina 40,000, wengi wao wakiwa watoto na kina mama na kuwajeruhi wengine zaidi ya 94,000, tangu kuanza kwa mashambulizi katika eneo la Gaza.