Naibu Rais Rigathi Gachagua na Waziri wa Uchukuzi na Barabara Kipchumba Murkomen leo Jumatatu wlitembelea kaunti ya Tana River kutathmini madhara yaliyosababishwa na mafuriko.
Tana River ni miongoni mwa kaunti zilizoathiriwa mno na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha nchini.
“Kama sehemu ya hatua zetu za kurejesha hali ya kawaida, nilitathmini kiwango cha uharibifu uliosababishwa na mvua za El Nino kwenye mto Tana,” alisema Naibu Rais.
“Rasilimali zimepelekwa na kazi inaendelea ya kuifanya kuwa sawa mitandao ya barabara na miundombinu mingine.”
Mafuriko yanayoshuhudiwa nchini Kenya kwa sasa yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 130 huku zaidi ya familia 90,000 zikiachwa bila makazi.
Mafuriko hayo aidha yamesababisha uharibifu wa barabara na kutatiza usafiri katika kaunti zilizoathiriwa mno.
Serikali inasema jumla ya kaunti 38 zimeathiriwa mno na mafuriko ikiwa ni pamoja na Mombasa, Mandera, Wajir, Isiolo na Makueni miongoni mwa zingine.