Home Habari Kuu Madereva watakiwa kuwa waangalifu msimu huu wa sherehe

Madereva watakiwa kuwa waangalifu msimu huu wa sherehe

0
Picha kwa hisani ya Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS

Mkewe Naibu Rais Dorcas Rigathi ametoa wito kwa madereva kuwa waangalifu msimu huu wa sherehe ili kuepusha maafa barabarani. 

Katika salamu zake za msimu wa sherehe kwa Wakenya, Dorcas aliwaonya madereva kutothubutu kuendesha magari wakiwa walevi.

“Nawataka kusalia makini ili tuweze kuwa na taifa lenye tija na maendeleo,” alisema mkewe Naibu Rais.

“Nawataka msherehekee mkiwa hai, kama ambavyo nimekuwa nikisema, nawataka msherehekee mtakavyo. Nawataka msherehekee mkiwa waangalifu.”

Alisikitika kwamba watu wengi wamelamazwa kupitia ajali za barabarani, kitu anachosema hakipaswi kutokea wakati wa msimu huu wa sherehe.

Kulingana naye, nyingi ya ajali hizo hutokea kwa sababu ya madereva kuendesha magari wakiwa walevi.

“Wakati unapoendesha gari, endesha usipokuwa mlevi. Tunapaswa kuwa waangalifu msimu huu. Tusije tukasababisha vifo wakati tunaweza tukajidhibiti.”

Matamshi yake yanawadia wakati ambapo kumekuwa na ongezeko la ajali ambazo zimesababisha vifo vya watu kadhaa na wengine kujeruhiwa kutokana na ajali za barabarani katika siku za hivi majuzi.

jana Jumatatu, watu wanne walifariki kwenye barabara ya Eldoret-Nakuru baada ya matatu kugongana na basi.

Abiria wengine 9 walijeruhiwa wakati wa ajali hiyo na kukimbizwa hospitalini ili kupokea matibabu.

Kule Makueni, ajali nyingine iliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita ilisababisha vifo vya zaidi ya watu 10 huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.

Wizara ya Barabara na Uchukuzi kwa sasa inaendesha kampeni kwa jina “Kampeni ya Usalama Barabarani Msimu wa Sherehe” inayolenga kuhamasisha watumiaji wa barabara kutahadhari ili kuepusha maafa zaidi barabarani.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, watu 3,999 walifariki mwaka huu kutokana na ajali za barabarani kati ya Januari 1 – Disemba 7,2023 ikilinganishwa na 4, 352 waliofariki mwaka uliotangulia.