Home Habari Kuu Madaktari Nyamira kupandishwa vyeo, wafutilia mbali mgomo

Madaktari Nyamira kupandishwa vyeo, wafutilia mbali mgomo

0

Madaktari katika kaunti ya Nyamira wamefutilia mbali ilani ya kufanya mgomo.  

Hii ni baada ya serikali ya kaunti hiyo inayoongozwa na Gavana Amos Nyaribo kuridhia matakwa yao ya kupandishwa vyeo.

“Madaktari katika kaunti ya Nyamira wamesitisha mgomo. Hii ni baada ya serikali ya kaunti ya Nyamira kuridhia matakwa yao ya kupandishwa vyeo. Serikali hiyo imeahidi kuwapandisha vyeo madaktari wake wote katika makubaliano ya pamoja, CBA yaliyotiwa saini kati yake na chama cha madaktari nchini, KMPDU Jumatano mchana,” ilisema taarifa kutoka kwa KPMDU.

Madaktari hao mnamo Septemba 4, 2023 walikuwa wametoa ilani ya siku 21 ya kufanya mgomo ikiwa utawala wa kaunti hiyo ungeyapa matakwao yao sikio la kufa.

Ilani hiyo ilichochea kuanza kwa mazungumzo kati ya utawala wa kaunti hiyo na madaktari hao kupitia chama chao cha KMPDU, maajadiliano ambayo hatimaye yamezaa matunda na kuepusha mgomo ambao wengi walihofia ungewaacha wagonjwa wengi taabani.