Home Habari Kuu Madaktari Nakuru waandamana kulalamikia kifo cha mwenzao

Madaktari Nakuru waandamana kulalamikia kifo cha mwenzao

0

Utoaji huduma katika hospitali ya rufaa ya Nakuru ulitatizika leo Jumatatu baada ya madaktari hospitalini hapo kuandamana kulalamikia kifo cha daktari mwenzao mwanagenzi. 

Mwili wa Dkt. Laban Langat ulipatikana na maafisa wa usalama ukiwa umetupwa kwenye mtaro nje ya hospitali hiyo juzi Jumamosi.

Maafisa wa kitengo cha upelelezi, DCI kwa sasa wanaendesha uchunguzi kubaini kilichosababisha kifo cha daktari huyo.

Hata hivyo, akiwahutubia wanahabari, katibu mkuu wa chama cha madaktari na wataalamu wa meno, KMPDU tawi la South Rift  Stephen Omondi aliwashtumu maafisa wa usalama katika kaunti ya Nakuru kwa utepetevu na kulalamikia kuzorota kwa hali ya usalama.

“Haja ya kuwakinga wahudumu wa afya dhidi ya kudhuriwa siyo tu hitaji la kimaadili bali ushuhuda wa ubinadamu wetu sisi sote,” alisema Omondi.

Madaktari hao wametishia kutorejea kazini hadi waliosababisha mauaji ya daktari huyo wakamatwe na kuwajibishwa kisheria.