Home Habari Kuu Maafisa washauriwa kuwa na utu wanapofurusha wananchi misituni

Maafisa washauriwa kuwa na utu wanapofurusha wananchi misituni

0
Soipan Tuya-Waziri wa Mazingira

Wizara ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabia  Nchi na Misitu imewaelekeza maafisa wa idara mbalimbali wanaotekeleza operesheni ya kufurusha watu kutoka msitu wa Mau wahakikishe utu wanapotekeleza kazi hiyo.

Kupitia taarifa iliyotiwa saini na Waziri Soipan Tuya, wizara hiyo imeelezea kwamba inafahamu fika kuhusu operesheni inayoendelea inayolenga kurejesha sehemu zilizoharibiwa za msitu wa Mau kupitia kukomesha uvamizi wa binadamu na ukataji miti.

Hata hivyo, Tuya ameonya maafisa wa kundi hilo wakiongozwa na kamishna wa eneo la Rift Valley dhidi ya vitendo ambavyo vitasababisha maafa, uharibifu wa mali na kufurushwa kwa jamii halisi za maeneo ya karibu na msitu wa Mau.

Waziri ameelezea pia kwamba kuna mipango ya kubainisha mipaka ya misitu na baadaye kuweka ua kupitia kwa ushirikiano wa serikali na washirika wengine kama hatua ya kuzuia uharibifu wa misitu siku za usoni.

“Kando na msitu wa Mau, operesheni ya kukomesha uhalifu wa misitu kama vile uvamizi, ukataji miti na uchomaji makaa itaendelezwa kwenye misitu yote nchini,” alisema Waziri Tuya.

Aliomba Wakenya kote nchini waendelee kuunga mkono mpango wa serikali wa kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuripoti visa vinavyochukuliwa kuwa uhalifu wa misitu kupitia nambari ya simu ya Wizara ya Mazingira ambayo ni, 0800724570.

Website | + posts