Home Kaunti Maafisa wakuu wa manunuzi warambwa Kilifi, watakiwa kwenda likizo

Maafisa wakuu wa manunuzi warambwa Kilifi, watakiwa kwenda likizo

0

Gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro amewataka maafisa wakuu wa manunuzi katika kaunti hiyo kwenda kwenye likizo ya kulipwa ya siku 90 wakati uchunguzi ukifanywa kuhusiana na mienendo yao. 

Hii inafuatia malalamishi kutoka kwa umma kuwa maafisa hao wanatatiza utoaji huduma na kushawishi utoaji zabuni katika kaunti hiyo.

Katika taarifa iliyosomwa kwa niaba yake na kaimu katibu wa kaunti hiyo Martin Mwaro, Gavana Mung’aro alisema ameteua kamati ya wanachama saba ya malalamishi ya manunuzi ambayo imetwikwa  jukumu la kukusanya malalamishi na kuwasilisha ripoti yake katika kipindi cha siku 60.

“Katika kipindi cha siku chache zilizopita, tumepokea taarifa za kutilia mashaka kutoka kwa umma zikiashiria kuwepo uwezekano wa kutotii kanuni zinazoongoza maadili na uadilifu wa maafisa wa umma zinazowahusu maafisa wanaosimamia manunuzi,” alisema Gavana Mung’aro.

Miongoni mwa maafisa waliotakiwa kwenda likizoni ni pamoja na Matano Riziki Choga, Evelyn Kache, Priscilla Munga, Rehema Luvuno, Andrew Kai na Michael Mwadali.

Wengine ni Mary Riziki, Mulanda Mazonga, Andrew Kithi, Rose Charo na Habel Humphrey.

Dickson Wekesa
+ posts