Home Habari Kuu Maafisa wakomesha mpango wa ulaghai wa ajira ughaibuni

Maafisa wakomesha mpango wa ulaghai wa ajira ughaibuni

0

Maafisa wa upelelezi wa jinai DCI jijini Nairobi jana walisitisha mpango wa ulaghai wa kusajili wakenya wanaotaka ajira ughaibuni na kukamata washukiwa watano.

Washukiwa hao ni Nick Van Opstal raia wa kigeni, Samuel Marigi, Patrick Wangai, Susan Oluoch na Christine Muthoni Wangechi na walikamatwa kufuatia habari zilizotolewa na wananchi kuhusu kampuni mbili walizoshuku.

Mawakala wa kampuni hizo Alhanawa Jobs na Supply Link Ventures Ltd walikuwa wamekusanya wakenya wanaosaka ajira kutoka Nairobi na viunga vyake katika uwanja wa KCB ambapo walidai kuwasajili na kuwasaidia kupata ajira hizo.

Wakenya wapatao 1000 waliokolewa kutokana na ulaghai huo wa watu ambao walikuwa na nia ya kuwatapeli.

Uchunguzi wa mwanzo ulionyesha kwamba mamlaka ya kitaifa ya ajira ilikuwa imetangaza mpango huo wa usajili kuwa usio halali.

Huku hayo yakijiri, maafisa wa usalama wanaendelea kuwasaka washukiwa wengine watatu ambao ni Hannah Mbugua, Gladys Oluasa na Lucy Wanjiru ambao walikwepa.

Wakenya wanahimizwa kuwa macho kila wakati na kuripoti visa vya utapeli kama hivyo.

Website | + posts