Home Kaunti Maafisa wakatili dhidi ya wanaotafuta kuni wamulikwa

Maafisa wakatili dhidi ya wanaotafuta kuni wamulikwa

Waziri wa afya Susan Nakumicha, Gavana wa kaunti ya Elgeyo marakwet Wisely Rotich na mbunge wa eneo la Keiyo Kaskazini Adams Kipsanai wamelalamikia ukatili wa maafisa wa kulinda misitu dhidi ya kina mama na wasichana wanaoingia kwenye msitu wa Kapchemutwa katika kaunti ya Elgeyo marakwet kutafuta kuni.

Viongozi hao walikuwa wakizungumza katika shule ya msingi ya Bugar iliyo katika kaunti ya Elgeyo marakwet wakati wa shughuli ya upanzi wa miche ya miti.

Waliitaka huduma ya misitu Kenya kutafuta namna ya kukubaliana na jamii zinazoishi karibu na misitu ili ziweze kupata kuni kutoka kwenye misitu hiyo bila adhabu kali wanayopata kila wanapofanya hivyo.

Viongozi hao walizungumzia kisa cha mama ya watoto 7 wa umri wa makamo kupoteza meno manne alipoanguka akiwa anakimbizwa na maafisa wa KFS baada ya kupatikana akikusanya kuni kwenye msitu huo.

Kuhusu kuvuna miti iliyokomaa kwenye misitu, viongozi hao walitaka jamii zilizo karibu na misitu zipatiwe kipaumbele kabla ya leseni kutolewa kwa wafanyabiashara wengine.