Maafisa wa utawala wa serikali ya kitaifa ambao zamani ulifahamika kama utawala wa mikoa ni muhimu kwa uongozi na maendeleo ya taifa hili.
Rais William Ruto has amesema maafisa hao ni nguzo muhimu kwa uthabiti wa taifa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kote nchini.
Hata hivyo, Rais amesema usalama wa kudumu na uthabiti wa nchi, na pia utekelezaji kwa ufanisi wa miradi ya maendeleo vinaweza tu kufikiwa ikiwa maafisa hao watafanya kazi zao kwa kujituma na kwa njia bora.
Ruto aliyasema hayo alipowahutubia maafisa hao katika Shule ya Serikali nchini, KSG katika eneo la Lower Kabete, kaunti ya Nairobi leo Jumanne.
Maafisa hao walijumuisha makamishna wa kikanda, makamishna wa kaunti na manaibu wao.
“Nataka kusema bayana leo kuwa nafasi yenu nchini ni ya kikatiba, halali na iliyo sawa. Sasa ni fursa yenu kuwatumikia Wakenya kwa uadilifu,” alisema Rais Ruto.
Aliwaambia maafisa hao kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono akiongeza kuwa wanafanya kazi kwa karibu na raia mashinani.
“Tutawaunga mkono na kuwawezesha kutoa uongozi katika maeneo yenu ya utawala na kusaidia kufungua uwezo wa Kenya.”
Kiongozi wa nchi aliwakumbusha maafisa hao kuwa wanahudumu katika nchi ambayo ina demokrasia thabiti akielezea kuwa utawala wa sheria na haki vinapaswa kuwaongoza katika utendakazi wao.
Wakati huohuo, Ruto aliwaagiza maafisa hao kuhakikisha wazazi wote katika maeneo yao ya utawala wanawapeleka watoto wao shuleni.