Naibu Rais Rigathi Gachagua ametoa onyo kali kwa maafisa wa usalama katika kaunti ya Kirinyaga, kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria, baada ya zaidi ya watu 10 kufariki walipokunywa pombe haramu.
Gachagua alisema serikali itaanzisha uchunguzi kuhusu maafisa wa usalama kutoka kaunti ya Kirinyaga badala ya kuwahamishia sehemu zingine.
“Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya maafisa wa serikali ya kitaifa na wale wa usalama ambao kupitia utepetevu au ufisadi, walifanikisha utengenezaji, usambazaji na uuzaji wa pombe haramu katika maeneo yao, kama ilivyofanyika Kirinyaga ambapo tulipoteza watu kupitia pombe yenye sumu,” alisema Gachagua.
Naibu huyo wa Rais alisema huku utawala wa Rais William Ruto ukijizatiti kupiga jeki uzalishaji bidhaa wa humu nchini, serikali haitakubali biashara ambazo zinahatarisha maisha ya wakenya.
“Huku biashara zikiimarisha uchumi wa taifa hili, hazipaswi kuhatarisha maisha ya wakenya,” alisema Gachagua.
Gachagua aliitaka idara ya mahakama kukoma kutoa maagizo ya kuzuia kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa wafanyibiashara walaghai.
Zaidi ya watu 10 walifariki na wengine kadhaa kupofuka baada ya kubugia pombe haramu kaunti ya Kirinyaga siku ya Jumatano.
Mmiliki wa eneo lililouza pombe hiyo anazuiliwa kwa siku 20 kusubiri kukamilishwa kwa uchunguzi.