Maafisa wa usalama katika kaunti ya Busia na sehemu zingine za nchi, wameagizwa kukabiliana vilivyo na majangili wanaowahangaisha wananchi.
Akitoa agizo hilo, waziri wa usalama wa taifa Prof. Kithure Kindiki alisema serikali haitavumilia magenge ya wahalifu huku akiwahakikishia wananchi usalama wao.
Waziri alisema serikali itabuni vituo zaidi vya utawala, ili kuleta huduma za serikali karibu na wananchi.
“Maafisa wote wa utawala lazima wawahudumie wakenya kwa kujitolea na kwa heshima,”alisema Waziri kindiki.
Aidha alisema afisa yoyote wa utawala atakayepatikana akiitisha hongo, hataachishwa tu, mbali pia atashtakiwa kwa mujibu wa sheria.
Wakati huo huo huduma katika afisi ya kaunti ndogo ya Teso zilizinduliwa, huku Jack Orare akiteuliwa kuwa naibu wa kwanza wa kamishna wa kaunti..