Serikali itawapeleka maafisa wa polisi katika viwanda vyote vya kahawa hapa nchini, kukabiliana na visa vinavyoongezeka vya wizi wa zao hilo, hayo ni kwa mujibu wa naibu rais Rigathi Gachagua.
Kulingana na naibu huyo wa Rais, wizi huo wa kahawa umesababisha hasara kubwa kwa wakulima, na wakati umewadia wa kuukomesha.
Aidha alikariri kujitolea kwa serikali kutatua changamoto zinazokumba sekta ya kahawa katika kipindi cha mwaka mmoja.
Akizungumza katika jumba la Wakulima jijini Nairobi ambako alizindua upya mnada wa kahawa wa Nairobi, Gachagua alitoa wito wa kuangaziwa upya sheria za kahawa na vyama vya ushirika ili kuziba mianya iliyopo katika usimamizi wa sekta hiyo.
Alisema marekebisho ya sera za kahawa yatatokomeza walaghai katika sekta hiyo ili kuhakikisha wakulima wananufaika na mazao yao.
Marekebisho ya sheria hiyo yanakusudiwa kukabiliana na maafisa watoro wa vyama vya ushirika wa kahawa wanaoshirikiana na mawakala walaghai hao kuwanyima wakulima faida.
Gachagua alisema serikali inakadiria kutenga fedha za kuwakinga wakulima kutokana na hasara katika kipindi hicho cha mwaka mmoja wakati marekebisho hayo yatakapokuwa yakitekelezwa.
Mnada wa kahawa wa Nairobi unarejelea shughuli zake baada ya kuafiki vigezo vilivyotolewa na halmashauri ya soko la mtaji.