Mamlaka huru ya kutathmini utendakazi wa polisi nchini IPOA imewaita maafisa wa polisi zaidi ya 50 kuhojiwa kuhusu visa vya mauaji, majeruhi na vingine vilivyotokea wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024.
Hatua hii inajiri baada ya lalama za wanaharakati wa kutetea haki pamoja na chama cha wanasheria nchini LSK kwamba polisi walihusika kwenye mauaji na utekaji nyara wa waandamanaji.
Stakabadhi za IPOA zinaonyesha kwamba maafisa wakuu wa polisi wapatao 15 ni kati ya polisi walioitwa na IPOA kuhojiwa kati ya Septemba 16 na 19, 2024.
Huduma ya taifa ya polisi ilielekeza maafisa hao kukutana na mawakili wao leo kabla ya kwenda kuhojiwa na IPOA.
IPOA ilimwandikia barua naibu inspekta jenerali wa polisi mnamo Agosti 30, 2024 kumfahamisha kuhusu uchunguzi huru uliokuwa ukiendelea kuhusu mauaji na majeruhi wakati wa maandamano.
Uchunguzi huo kulingana na IPOA ulifichua kwamba maafisa kadhaa wa polisi walihusika na vitendo vya kikatili wakati wa maandamano ya Gen Z na ya muungano wa Azimio mwaka jana.