Home Habari Kuu Maafisa wa KPA wakamatwa, wafikishwa mahakamani kwa tuhuma za ufisadi

Maafisa wa KPA wakamatwa, wafikishwa mahakamani kwa tuhuma za ufisadi

0

Washukiwa 9 wakiwemo maafisa 6 wa Halmashauri ya Bandari Nchini, KPA wamekamatwa kuhusiana na tuhuma za ufisadi unaohusisha zabuni ya shilingi milioni 62. 

Tisa hao walikamatwa na wapelelezi kutoka Afisi ya Kanda ya Mombasa ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC.

“Washukiwa kwa sasa wamefikishwa katika mahakama ya kupambana na ufisadi ya Mombasa leo asubuhi,” ilisema EACC katika taarifa.

Tume hiyo ikisema uchunguzi ulibaini washukiwa hao walitekeleza njama ya ulaghai wa kupora fedha za umma kupitia zabuni iliyotolewa kwa kampuni walio na uhusiano nayo.

Watashtakiwa kwa kuwa na mkinzano wa maslahi, kujipatia mali ya umma kwa ulaghai na kughushi nyaraka zilizotumika katika njama hiyo.