Home Habari Kuu Maafisa wa kliniki wagoma

Maafisa wa kliniki wagoma

0

Muungano wa Maafisa wa Kliniki (KUCO) ulitangaza kwamba mgomo ungeanza jana Jumatano usiku wa manane katika hospitali zote za umma.

KUCO ilitangaza hayo Jumatano kupitia ujumbe kwenye mtandao wa X ikisema kwamba ilichukua uamuzi huo kufuatia onyo la Mahakama ya Ajira na Mahusiano ya Kazi (ELRC) kwa kaunti dhidi ya kunyanyasa maafisa wa kliniki ambao wangeshiriki mgomo.

“Mgomo wetu umelindwa, mahakama ilisisitiza hili kwa kulinda wanachama wetu dhidi ya unyanyasaji au michakato ya kinidhamu na Kaunti 47 na Wizara ya Afya. Wakati huo huo, tunaondoa Maafisa wa Kliniki wote kutoka kwa vituo vya afya kuanzia usiku wa manane leo,” KUCO ilitangaza katika taarifa.

Vituo vyote vya afya vya umma vimeathirika na mgomo huo hivyo basi kuwaumiza wananchi kote nchini hususan wale wasioweza kumudu gharama ya hospitali za kibinafsi.

Maafisa wa kliniki wanashiriki mgomo huu kwa mara ya kwanza nchini. ELRC ilitoa notisi ya kuwalinda maafisa hao wa kliniki siku moja baada ya mazungumzo na magavana kusambaratika baada ya wakuu wa kaunti kusema kuwa Makubaliano ya pamoja ya mazungumzo (CBA) ilitiwa saini na serikali ya kitaifa wala sio vitengo vya ugatuzi.

“Pande zote ziendelee kuelekea mazungumzo ya kusuluhisha mgogoro huo kwa nia njema kwa kila mkutano uliopangwa kufanyika Mei 14, na baada ya hapo kama inavyofaa,” ELRC iliagiza.

KUCO inataka maafisa wa kliniki waidhinishwe kuwa wafanyikazi wa kudumu na pensheni, ikisema kuwa wakati Wizara ya Afya iliashiria utayari wa bajeti, iliongeza kandarasi za Huduma ya Afya kwa Wote (UHC) chini ya masharti yanayogandamiza.

Muungano huo pia ulishutumu Baraza la Magavana (CoG) kwa kukataa kuafikia makubaliano. KUCO inasema kuwa CoG iliongeza kandarasi za UHC chini ya masharti yanayogandamiza.

Mgomo huu unajiri wakati mgomo wa matabibu ukifika siku ya 45. Matabibu hao wanadai kuhitimishwa kwa mazungumzo ya muda mrefu juu ya Mkataba wake wa Makubaliano ya Pamoja (CBA), mazungumzo ambayo yalikwama tangu mwaka wa 2017.

Alphas Lagat
+ posts