Home Habari Kuu Maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani

Maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani

0

Siku ya Redio Duniani inaadhimishwa leo Jumanne, Februari 13, 2024 huku wadau katika sekta ya mawasiliano wakiangazia mchango wa redio kama chombo cha mawasiliano katika ustawi wa jamii. 

Siku ya Redio Duniani huadhimishwa Februari 13 kila mwaka.

Siku hiyo ilitangazwa na nchi wanachama wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO mnamo mwaka 2011. Kisha siku hiyo iliidhinishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo Januari 14, 2013 kuwa siku ya kimataifa.

“Wakati wa Siku hii ya Redio Duniani, tunasherehekea siyo tu historia ya redio, lakini pia wajibu wake muhimu katika jamii zetu, kwa sasa na katika miaka ijayo,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay.

Maudhui ya maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani mwaka huu ni “Historia yenye tija ya redio, umuhimu unaoendelea, na siku za usoni zenye matumaini.”

Redio kama chombo cha mawasiliano imekuwa ikitumika kwa kipindi cha miaka 100 iliyopita sasa.

Humu nchini, redio imetumika kama chombo muhimu cha kuwataarifu, kuwaelimisha na kuwaburudisha wasikilizaji wake.

Idhaa ya Redio Taifa inayomilikiwa na shirika la utangazaji nchini, KBC imekuwa katika mstari wa mbele kuwatumbuiza wasikilizaji wake kila pembe ya nchi sawia na idhaa zingine za KBC zinazotangaza katika lugha ya mama kama vile Radio Mayienga, Radio Ingo, Coro FM, na Kitwek miongoni idhaa zingine nyingi za shirika hilo.

Kenya kwa sasa ina zaidi ya vituo 100 vya redio, na idadi ya vituo vinavyomilikiwa na watu binafsi na mashirika inaendelea kuongezeka.

Hata hivyo, ingawa umuhimu wake katika jamii unasalia kuwa imara, redio kama chombo cha mawasiliano imekumbana na ushindani mkali kutoka kwa mifumo ya dijitali na mitandao ya kijamii kama vile Facebook, X zamani ukijulikana kama Twitter, YouTube na Instagram miongoni mwa mingine.

Hali hii imesababisha kupungua kwa mapato kwa kiwango kikubwa na hivyo kuathiri mno utendakazi wake.

Katika hali zingine, kunayo mashirika ambayo yamelazimika kuwafuta kazi baadhi ya wafanyakazi wake kutokana na uhaba wa fedha za kugharimia malipo yao.

Licha ya changamoto hizo, wengi wanakisia kuwa redio itastahimili mawingi ya changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya kasi ya teknolojia na kuendelea kuwa chombo cha kutegemewa cha mawasiliano katika kuwataarifu, kuwaelimisha na kuwaburudisha wasikilizaji wake.

 

Website | + posts