Home Burudani Lupita Nyong’o ateuliwa kiongozi wa jopo la waamuzi la tamasha ya filamu...

Lupita Nyong’o ateuliwa kiongozi wa jopo la waamuzi la tamasha ya filamu ya Berlin

0

Lupita Nyong’o mwigizaji wa asili ya Kenya na mshindi wa tuzo ya Oscar, ameteuliwa kuongoza jopo la waamuzi wa tamasha ya filamu ya kimataifa ya Berlin inayoanza wiki hii nchini Ujerumani.

Amevunja rekodi ya kuwa mtu wa kwanza mweusi kuwahi kushikilia wadhifa huo katika historia ya miaka 74 ya jopo hilo.

Kila mwaka, tamasha ya filamu ya Berlin huteua kiongozi mpya.

Wakurugenzi wa tamasha hiyo ya filamu Mariëtte Rissenbeek na Carlo Chatrian, walitetea uteuzi wa Lupita wakisema anawakilisha uwezo mkubwa wa kukumbatia majukumu tofauti yanayolenga hadhira tofauti.

Bi. Nyong’o ataongoza mchakato wa uteuzi wa filamu mbili zitakazoshinda katika vitengo viwili vikuu ambavyo ni Golden Bear na Silver Bear.

Wakati wa ufunguzi wa hafla hiyo, Lupita alisema anahisi ametunukiwa heshima kwa kuteuliwa akisema utofauti kati ya wanajopo utaboresha mchakato wa kuchagua filamu bora.

Filamu tatu kutoka Afrika ni kati ya 20 zilizoorodheshwa kuwania tuzo kuu na zinasimulia hadithi muhimu za bara hili.

Zinafahamika kama “Black Tea” ya mwelekezi wa Mauritius na Malia Abderrahmane Sissako, “Who Do I Belong To” ya mwelekezi wa Tunisia na Canada Meryam Joobeur na filamu ya matukio halisi “Dahomey” ya Mati Diop wa Ufaransa na Senegal.

Matamasha makuu ya filamu ulimwenguni yanayojumuisha Berlin, Cannes, Venice, Sundance na Toronto yamekuwa yakikosolewa kwa miaka mingi kwa kukosa wawakilishi wa sehemu nyingine za ulimwengu.

Tamasha ya Cannes ilipata kiongozi wa kwanza mweusi mwaka 2020, wakati mwelekezi Spike Lee aliteuliwa.