Home Habari Kuu LSK yapinga mkutano kati ya Rais Ruto na Jaji Mkuu Koome

LSK yapinga mkutano kati ya Rais Ruto na Jaji Mkuu Koome

0

Chama cha mawakili nchini, LSK kimepinga kufanyika kwa mkutano kati ya Rais William Ruto na Jaji Mkuu Martha Koome.

Akiwahutubia wanahabari juzi Jumatatu, Jaji Koome aliiongoza tume ya huduma za mahakama, JSC kuashiria kuwa wako tayari kukutana na Rais Ruto ili kuangazia madai kuwa ufisadi umekithiri katika idara ya mahakama.

Rais Ruto ameridhia wito huo.

Hata hivyo, chama cha LSK kupitia kwa mwenyekiti wake Eric Theuri kimetoa wito kwa Jaji Koome kutoshiriki mkutano wowote na Rais Ruto.

“Tulitoa wito kwa Jaji Mkuu kutoshiriki majadiliano yoyote na uongozi mkuu wa nchi. Kuitikia kufanya majadiliano na uongozi mkuu wa nchi ni sawia na kujiingiza katika mapatano na ni kinyume cha katiba,” alisema Theuri wakati wa maandamano ya mawakili yaliyofanyika mjini Mombasa kuunga mkono idara ya mahakama.

“Nchi nzima itamhukumu vikali Jaji Mkuu ikiwa atashiriki majadiliano hayo. Hii itashusha zaidi imani ya umma katika idara ya mahakama na kuhalalisha madai ya ufisadi na kufikia mapatano.”

Upinzani ukiongozwa na kiongozi wa muungano wa Azimio Raila Odinga pia umepinga kufanyika kwa majadiliano hayo.

Rais Ruto katika siku za hivi karibuni ameiongoza serikali ya Kenya Kwanza katika kuishutumu idara ya mahakama akisema imejaa na uvundo wa ufisadi.

Anaituhumu kwa kushirikiana na watu fulani kuhujumu mipango ya serikali kama vile mpango wa nyumba za bei nafuu.