Maafiswa wa usalama wamelinasa lori moja, nambari ya usajili KDG 044T, ambalo lilikuwa likisafirisha kemikali ya ethanol kwenye barabara ya Mzee wa nyama katika kaunti ya Nakuru.
Operesheni hiyo kali iliyopewa jina “operesheni usalama” iliendeshwa na maafiswa mbalimbali wakiwemo wale kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI, na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini, KRA.
Baada ya kulikagua lori hilo, maafisa walibaini kuwa lilibeba mapipa 22. Mapipa 16 yalikuwa na kemikali ya ethanol huku mengine 6 yakiwa tupu.
Thamani ya kemikali hiyo ilikadiriwa kuwa milioni 9.6 huku KRA ikipoteza kodi yenye thamani ya shilingi milioni 4.7.
Dereva wa lori hilo kwa jina Peter Karimi Kiarie anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Nakuru akisubiri kufunguliwa mashtaka.
Uchunguzi kuhusiana na biashara hiyo ya kimagendo bado unaendeea.