Home Burudani Lizzo ashtakiwa na waliokuwa wacheza densi wake

Lizzo ashtakiwa na waliokuwa wacheza densi wake

0

Mwanamuziki wa mtindo wa Pop Melissa Viviane Jefferson, maarufu kama Lizzo ameshtakiwa na watu watatu ambao awali walifanya naye kazi kama wanenguaji.

Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani jana Jumanne nao Arianna Davis, Crystal Williams na Noelle Rodriguez na kati ya makosa ambayo amelimbikiziwa ni unyanyasaji wa kingono, kidini na ubaguzi wa rangi.

Watatu hao wanadai kwamba wakati wakifanya kazi na Lizzo, walilazimishwa kutenda vitendo vya kudhalilisha kingono kati ya mwaka 2021 na 2023.

Arianna Davis anasema wakati mmoja alilazimishwa kushika matiti ya mcheza densi mwingine katika sehemu moja ya burudani mjini Amsterdam. Anasema alikataa mara ya kwanza lakini akalazimika kukubali kwa kuhofia hali yake siku za usoni kwenye kundi hilo la wacheza densi.

Lizzo ambaye ni mnene na husifia sana mwili wake anadaiwa pia kumdhalilisha Davis kuhusu mwili wake. Yeye na mwalimu wake wa densi Tanisha Scott, wanasemekana kumwingilia sana Davis wakati alionekana kuongeza uzani wa mwili. Walisisitiza awaeleze ikiwa alikuwa akipitia jambo gumu ambalo lilimfanya anenepe.

Kiongozi wa kundi hilo la wacheza densi wa Lizzo aitwaye Shirlene Quigley, naye analaumiwa kwa kulazimisha wacheza densi kukubali mafundisho ya dini yake ya Kikristo. Alizomea waliojihusisha na ngono kabla ya ndoa na akatoa hadharani habari kuhusu mmoja wa wacheza densi wao wa awali kuhusu ubikira wake.

Wacheza densi weusi wanasemekana kubaguliwa kwenye kundi hilo huku wakisingiziwa kuwa wavivu, wasiojua kazi yao na kuwa na mitazamo mibaya.

Davis, Williams na Rodriguez wanasema pia kwamba hawakulipwa vizuri wakati wa ziara ya Lizzo nchini Uingereza kwani walilipwa asilimia 25 tu ya marupurupu waliyokubaliana wakati ambapo hawakuwa jukwaani.

Davis na Williams walifutwa kutoka kundi hilo huku Rodriguez akijiuzulu ili kuunga mkono wenzake.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here