Viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania kiitwacho Chasema wameachiliwa kwa dhamana kulingana na taarifa ya msemaji wa chama hicho.
Tundu Lissu mmoja wa viongozi wa chama cha Chadema na wenzake walikamatwa jana Jumatatu walipokuwa wakijiandaa kwa mkutano wa siku ya vijana.
Inaripotiwa kwamba watu wapatao 520 walikamatwa katika sehemu mbali mbali za nchi ya Tanzania kabla ya mkutano huo ambao ulikuwa tayari umepigwa marufuku.
Mkutano huo ulitarajiwa kuhudhuriwa na vijana wengi katika mji wa Mbeya ulioko kusini magharibi mwa Tanzania.
Makundi ya kutetea haki za binadamu nchini humo yalikashifu kukamatwa kwa watu hao wakihofia kurejea kwa sera kandamizi zilizokuwepo wakati wa hayati John Magufuli.
Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, naibu wake Tundu Lissu, John Mnyika na John Pambalu ni kati ya walioachiliwa na kurejeshwa jijini Dar es Salaam na polisi.
Chadema imesema baadhi ya viongozi bado wako mikononi mwa polisi lakini haijatoa maelezo zaidi.
Afisi za chama hicho mjini Mbeya zinasemekana kuzingirwa na maafisa wa polisi ambao hawaruhusu yeyote kuingia huku polisi wakionya kwamba yeyote atakayejaribu kuvuruga amani atachukuliwa hatua kali kisheria.
Wanachama wa Chadema wanalaumiwa kwa kile kilichotajwa kuwa kupanga maandamano yenye vurugu.