Home Kimataifa Kuria: Niko tayari kufanya kazi katika wizara yoyote

Kuria: Niko tayari kufanya kazi katika wizara yoyote

0
kra

Waziri wa utumishi wa umma Moses Kuria amesema kwamba yuko tayari kufanya kazi katika wizara yoyote atakayoteuliwa na Rais kumsaidia kujenga nchi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.

Waziri huyo amesema anaondoka kwenye wizara ya biashara akijivunia mengi aliyofanikisha akiwa huko kama kuanzisha maeneo 15 ya viwanda katika sehemu mbali mbali nchini katika muda wa mwaka mmoja uliopita.

kra

Kuria, ambaye hadi jana alikuwa waziri wa biashara na uwekezaji, alikuwa akizungumza katika kaunti ya Garissa kwenye hafla ya kuzindua eneo la viwanda, ambalo ndilo la kwanza kabisa katika eneo la kaskazini mashariki tangu Kenya ilipopata Uhuru.

Huku akisisitiza kwamba bidii aliyokuwa nayo katika wizara ya biashara itadhihirika katika wizata ya utumishi wa umma, waziri Kuria alisema kwamba wote wana wajibu wa kusaidia Rais katika wadhifa wowote.

Katika wadhifa wake mpya Kuria anahimiza watendakazi wote wa umma na wanakandarasi wa serikali watoe huduma kulingana na mikataba yao ya kazi au waondoke kupisha watu waliohitimu wachukue nafasi zao.

Kuria ameahidi kujibidiisha kulainisha utoaji huduma katika sekta ya utendakazi wa umma akionya kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya afisa yeyote ambaye hataafikia lengo lake kikazi.

Alisema iwapo wanakandarasi hawatakamilisha miradi kwa wakati uliowekwa atatumia vijana kutoka huduma ya vijana kwa taifa NYS kukamilisha miradi hiyo.

Kulingana na Kuria asilimia 32 ya watendakazi wa umma wanastaafu katika muda wa miaka miwili hadi mitano ijayo na wataruhusu wanaotaka kustaafu walio na umri wa zaidi ya miaka 50 kufanya hivyo.

Website | + posts