Uongozi wa chama cha Walimu wa shule za sekondari na vyuo KUPPET umeapa kuendelea na mgomo wa kitaifa siku ya Jumatatu ambayo itakuwa wiki ya pili ya walimu kususia masomo tangu muhula wa tatu kung’oa nanga.
Kwenye kikao na wanahabari Jumapili,Katibu Mkuu wa KUPPET Akelo Misori amesema kuwa tume ya kuwaajiri walimu TSC, imepuuza mapendekezo ya wizara ya Leba na kuwalazimu kuendelea na mgomo wa kitaifa.
Misori ameishutumu TSC kwa kutumia ubabe badala ya kuzungumza na walimu na kusaini mwafaka wa kurejea kazini.
KUPPET imeitaja hatua ya TSC kuwapuuza walimu na kukataa kuzungumza nao kuwa kejeli na kumtaka Rais Ruto kuingilia kati.
Wanafunzi wa kidato cha nne wameratibiwa kuanza mtihani wa kitaifa KCSE mwezi ujao.
KUPPET imeapa kuendelea na mgomo wao hadi pale serikali itakapotimiza matakwa yote .