Home Kaunti Kupotea kwa punda kwalemaza biashara Limuru

Kupotea kwa punda kwalemaza biashara Limuru

0

Biashara ililemazwa kwa muda leo katika soko la nguo kuu kuu la Limuru kaunti ya Kiambu, baada ya wanaosafirisha nguo hizo hadi kwa wauzaji kukosa punda ambao huwa wanawatumia kwa usafirishaji.

Inasemekana punda hao wanaibwa na baadaye kuchinjwa kinyume cha sheria katika kaunti ndogo ya Ndeiya eneo bunge la Limuru.

Wasafirishaji hao wanalaumu biashara ya nyama na ngozi ya punda kwa masaibu yao wakisema imekithiri katika eneo hilo na wamepoteza wanyama ambao huwasaidia kubeba mizigo hiyo ambayo ni zaidi ya kilo 100 kwa wakati mmoja.

Sasa wanataka maafisa wa usalama kutekeleza msako katika eneo hilo

Mmoja wao kwa jina Man Yori Yori Mitumba anaitaka wizara ya biashara kwa ushirikiano na ile ya mambo ya nje kuchunguza wanaouza bidhaa za Kenya katika nchi kama China na nyingine.

Nchi hizo zinaaminika kuwa na mahitaji ya kiwango cha juu ya ngozi suala ambalo linahatarisha uwepo wa mnyama huyo muhimu ambaye ana uwezo wa kuzaa mara moja tu kwa mwaka.

Mshirikishi wa soko hilo la Limuru John Maina amenyoosha kidole cha lawama kwa maafisa katika kituo cha polisi cha Ndeiya ambao anasema wamelemaza juhudi zao za kunasa gari wanaloamini linatumika kusafirisha bidhaa hiyo.

Amemtaka kamanda wa polisi katika kaunti ya Kiambu aanzishe uchunguzi na kuhoji maafisa wa kituo hicho wanaoshukiwa kulinda wahalifu.

Kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Limuru Philip Mwania amesema doria zitaimarishwaakiomba wamiliki wa punda kuwalinda ipasavyo.

Website | + posts