Mamlaka ya Kuangazia Utendakazi wa Polisi, IPOA imeanzisha uchunguzi kuhusiana na madai kuwa maafisa wawili wa ulinzi wa Jaji Lawrence Mugambi wameondolewa.
Tume ya Huduma za Mahakama, JSC jana Jumatatu iliutaarifu umma kuwa maafisa hao waliondolewa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika taarifa, Mkurugenzi na Afisa Mkuu Mtendaji Elema Halake amesema IPOA tayari imeanzisha uchunguzi kuhusiana na madai hayo.
“Kwa kuzingatia madai hayo, IPOA, kwa hiari yake yenyewe, imeanzisha uchunguzi kuhusiana na madai ya kuondolewa kwa maafisa hao kwa mujibu wa sehemu ya 6 ya Sheria ya Mamlaka Huru ya Kuangazia Utendakazi wa Polisi, Kifungu 86 cha Sheria za Kenya,” alisema Halake katika taarifa.
“Uchunguzi huo utasaidia katika kutoa mapendekezo, ikiwa ni pamoja na siyo tu yanayohusiana na kufunguliwa kwa mashtaka, pale ambapo makosa yamebainika kufanywa.”
IPOA imetoa taarifa hiyo wakati ambapo Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Gilbert Masengeli amekanusha madai kuwa walinzi Jaji Mugambi wameondolewa.
Ametaja madai ya JSC kuwa yenye nia mbaya.
Maafisa wawili wa ulinzi wa Jaji Mugambi waliondolewa siku chache baada ya Jaji huyo kutoa uamuzi wa kumtaka Masengeli akamatwe kwa kuidharau mahakama.
JSC imetaja hatua hiyo kuwa yenye nia ya kumtisha Jaji Mugambi kufuatia uamuzi huo.
Madai ambayo Masengeli ameyapuuzilia mbali.
“Katika kisa cha Jaji Mugambi, maafisa hao wawili wa usalama ni maafisa kutoka huduma ya kawaida na kwa hivyo waliondolewa ili kushiriki mafunzo ya usalama wa viongozi mashuhuri, na mahali pao palichukuliwa na maafisa wa ulinzi wa viongozi mashuhuri kutoka kitengo cha polisi wa idara ya mahakama,” alisema Masengeli katika taarifa.
“Wajibu wa Inspekta Jenerali wa kulinda nchi ni mkubwa zaidi na kazi ya polisi ni ya kipekee. Ni wazi kwa umma kuwa wakati IG alipotakiwa kufika mbele ya mahakama, alikuwa anatathmini hali ya usalama katika maeneo ya Pwani na Kaskazini Mashariki. Kwa kutii agizo la mahakama, IG aliwakilishwa na Naibu IG wa Huduma ya Polisi nchini kwa sababu suala lililozungumziwa halikumhusu IG binafsi.”
Masengeli ametakiwa mara kadhaa kufika mbele ya mahakama kuelezea waliko wanaharakati watatu wanaodaiwa kukamatwa na polisi karibu mwezi mmoja uliopita.
Hata hivyo, amekaidi agizo la kufika mahakamani, hali ambayo ilimlazimu Jaji Mugambi kutoa uamuzi wa kukamatwa kwake kwa kuidharau mahakama.